Yanga wanaendelea kumkosa Ajib
Kikosi cha Yanga sasa kimesafiri kuelekea Mtwara kucheza mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Ndanda FC Wanakuchele, wakiwa na jumla ya wachezaji 20 na benchi lao la ufundi, mchezo kati ya Yanga na Ndanda utachezwa katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Aprili 4.
Msemaji wa Yanga Dismas Ten amethibitisha taarifa hizo kuwa pamoja na kutajwa kikosi cha wachezaji 20 lakini wataendelea kumkosa nahodha wa timu hiyo Ibrahim Ajib anayeendelea kuuguza majeraha yake.
“Ibrahim Ajib bado tutaendelea kumkosa kikosini kutokana na majeraha ya
mguu,lakini jambo jema ni kwamba Juma Abdul amerejea kikosini na atakuwa
sehemu ya msafara wa kikosi chetu,mchezo utakuwa mgumu lakini maandalizi
tuliyoyafanya yanatosha kutupa matokeo mazuri”. Alisema Dismas Ten kupitia Yanga TV
Yanga wana-uchu wa kurejesha taji walilolipoteza kwa watani zao Simba SC msimu uliopita, japokuwa Simba ameonekana kuwa makini na viporo na anaweza akavuna alama zote za viporo, Yanga anaongoza TPL kwa kuwa na alama 67, akicheza michezo 28 akifuatiwa na Azam FC walio na alama 59 wakiwa na michezo 28 na Simba SC nafasi ya tatu akiwa na alama 57 akicheza michezo 22 hivyo ana viporo 6.