Amunike ampakulia nyama Fei Toto
Tukiwa tunaelekea katika maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika nchini Misri AFCON 2019, kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars raia wa Nigeria Emmanuel Amunike amesimama na kumsifia kiungo wa Yanga na Taifa Stars Feisal Salum kwa kiwango anachoendelea kukionesha.
Amunike amemsifia sana Feisal kwa lugha ya mtaani wanasema amempakulia nyama kutokana na uwezo wa nyota huyo akiwa bado ana umri mdogo.
.
Amunike amesifia kiasi cha kueleza kuwa Feisal Salum kama angekuwa Ulaya basi angekuwa anacheza soka katika timu kama FC Barcelona. .
“Sio kila mchezaji ambaye ni mzuri katika Ligi ni mzuri katika timu ya taifa, katika Ligi unacheza kila Jumapili na unasubiri tena Jumapili ijayo una muda lakini katika timu ya taifa unacheza siku mbili au tatu unashindana hivyo tunahitaji wachezaji wanaoweza kushindana, Feisal sio mtoto mdogo anaweza kupambana, angekuwa Ulaya angeweza kucheza timu kama Barcelona” alisema Amunike kwenye mahojiano na Mtanzania Digital
Tukukumbushe tu Emmanuel Amunike (48) alikuwa mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria na amewahi kucheza soka katika kiwango cha juu akiwa katika vilabu tofauti tofauti Ulaya, kama FC Barcelona ya Hispania inayochezewa na Lionel Messi kwa sasa na klabu ya Sporting Lisbon ya Ureno iliyomlea na kumuibua nyota wa Juventus Cristiano Ronaldo.