Wachezaji wa Bolton wagoma kisa Mshahara
Wachezaji wa klabu ya Bolton inayoshiriki ligi ya Championship nchini England leo wameanza mgomo wa kutokwenda mazoezini mpaka pale wao na wafanyakazi wa klabu watakapolipwa mishahara ya mwezi Machi.
Mishahara yao ya mwezi walitakiwa kulipwa Ijumaa iliyopita Machi 29, lakini mpaka leo jumatatu mchana akaunti zao hazipata chochote.
Huu ni mwezi wa pili mfululizo wanacheleweshewa mishahara yao. Mwezi Februari mishahara ilichelewa kwa muda wa siku 10.
Mmiliki wa klabu hiyo Ken Anderson jumatano iliyopita aliwaambia wafanyakazi wa klabu hiyo kuwa yupo katika hatua za mwisho kuiuza timu hiyo na kuwaambia ndani ya saa 48 zinazofuata dili hilo litakuwa limekamilika ,lakini hakuna kilichotimia mpaka sasa.
Timu hiyo inaandamwa na madeni pamoja na malimbikizo ya kodi ambayo yanafikia Pauni Milioni 1.2 , na Machi 30 mwaka huu mahakama ilitoa wiki mbili timu hiyo iwe imelipa madeni hayo.
Bolton wapo katika nafasi ya kushuka daraja, sasa wanashika nafasi ya 23 katika Championship zikiwa zimebaki mechi saba msimu kumalizika.