Pique arejea timu ya Taifa kwa sura nyingine
Beki wa klabu ya FC Barcelona ya nchini Hispania Gerard Pique baada ya kutangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Hispania mwaka uliyopita baada ya Kombe la Dunia 2018, amerudi tena kucheza soka la kimataifa safari hii akiichezea timu ya taifa ya jimbo la Catalunya ambayo mara kadhaa imekuwa ikishinikiza kutaka kutambulika kama nchi na kujitenga na Hispania.
Mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Venezuela ulifanikiwa kumalizika kwa Catalunya kupata ushindi wa mabao 2-1 .
Mchezo huo ambao ulichezwa siku ya jumatatu mjini Girona, haukuwa na waamuzi rasmi kwa sababu haukuwa unatambulika na FIFA au UEFA.
Mechi hiyo ya kirafiki Catalunya ambao wanapigania kwa sasa kupata uhuru wao na kujitenga na Hispania ili watambulike kama taifa huru, waliwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na vilabu vinavyomiliki wachezaji hao visivyo ndani ya jimbo la Catalunya kugoma kuwaruhusu kwa kuhofia wanaweza kupata majeruhi na kushindwa kurudi kuvitumikia vilabu vyao katika michezo ya Ligi Kuu nchini Hispania.