Azam fc wajifunza kutokana na makosa
Klabu ya Azam FC yenye maskani yake Mbande Chamazi jijini Dar es Salaam inaonekana imejifunza kitu baada ya awali kuwahi kudaiwa kufanya makosa kuwaachia wachezaji wake nyota kama John Bocco, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Aishi Manula waondoke bure kutokana na kutofikia nao makubaliano katika maslahi binafsi.
Nyota hao waliondoka kwa mpigo na kujiunga na Simba SC ambapo wakiwa kwenye msimu wao wa kwanza wakaiwezesha Simba SC kuchukua Ubingwa wa ligi, hivyo unaweza kusema kuwa Azam FC ni kama waliwaachia maadui zao wanaocheza nao Ligi Moja silaha za kivita, hilo kwa mujibu wa wachambuzi wengi linadaiwa kuwa kosa kubwa kuwahi kufanywa na klabu hiyo.
Afisa mtendaji mkuu wao wa sasa Abdulkarim Amin ‘Popat’ ameonekana kujizatiti mapema kwa kuwaongezea mikataba wachezaji wake watatu Donald Ngoma Machi 14 kasaini mkataba mpya wa mwaka mmoja, Bruce Kangwa Machi 21 amesaini kandarasi mpya ya miaka miwili na sasa wamemuongezea tena Abdallah Kheri mkataba mpya wa miaka mitatu baada ya mkataba wake wa sasa kuwa ulikuwa unatarajiwa kumalizika Mei mwaka huu.
Mkataba mpya wa Abdallah Kheri ‘Sebo’ utamuweka kwa wababe hao wa Chamazi hadi 2022, hiyo ikizidi kuonesha kuwa Azam FC hawataki kupoteza wachezaji wao muhimu wa kikosi cha kwanza kwa mkupuo kama walivyokosea msimu wa mwaka juzi, ndio maana ndani ya wiki mbili imewaongezea mikataba wachezaji wake watatu.