Sir Alex arudisha fadhila baada ya kupona Ubongo
Ni furaha kwa wanamichezo wengi duniani kumuona kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson ambaye anatajwa kama miongoni mwa makocha bora waliowahi kutokea akiwa sawa kiafya pamoja na kuwa kwa sasa amebaki kama shabiki tu wa mchezo wa soka baada ya kustaafu.
Dunia ya soka mwaka uliopita ulizipokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kuumwa ghafla kwa Sir Alex Ferguson na kulazimika kufanyiwa upasuaji katika ubongo (Brain Haemorrhage) ambao unatajwa kuwa ni sehemu hatari kwa kufanyiwa upasuaji na huwa inahitaji umakini mkubwa.
Kocha huyo ambaye ana umri wa miaka 77 kwa sasa baada ya afya yake kuimarika na kurudi katika hali yake ya kawaida, amefanikiwa kuchangisha (charity event) pauni 405,000 (Tsh bilioni 1.2) na kuzipeleka katika mfuko wa taifa wa huduma za afya (NHS) kama shukrani kwa upasuaji wa ubongo wake kwa usalama.
Katika tukio hilo la uchangiaji liliofanyika Manchester Hotel ijumaa usiku likiongozwa mwigizaji James Nesbitt, kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alikuwa ni miongoni mwa waliohudhuria
Sir Alex Ferguson ambaye ni raia wa Scotland ni miongoni mwa makocha bora na katika maisha yake ya ufundishaji soka kwa miaka 26 akiwa na Manchester United amefanikiwa kushinda jumla ya mataji 38, pamoja na kustaafu Ferguson amekuwa akionekana katika mechi mbalimbali za Manchester United.