Shujaa wa 1979 Ndola ni Joel Bendera, Shujaa wa kesho Temeke ni wewe Mtanzania
Joel Bendera ndiye shujaa aliyeipeleka Tanzania katika michuano ya AFCON mwaka 1980, hayo ni maneno ya nyota wa zamani wa Taifa Stars Peter Tino.
Agosti 26, 1979 Tanzania ilikuwa inahitaji sare yoyote tu mjini,Ndola Zambia ili ifuzu kwenye michuano ya AFCON 1980 Nigeria, Hii ni baada ya kushinda goli 1-0 jijini Dar es salaam uwanja wa Uhuru katika mchezo wa kwanza.
Wanafika Zambia, Taifa Stars walipelekwa katika ubalozi wa Tanzania, Balozi hakuwapa chai wala maandazi, ila aliwapa magazeti ya Zambia wayaone, magazeti yale ndio yaliwatia hasira ya kutaka kwenda Nigeria, magazeti yalimuonesha Rais wa Zambia kipindi hicho Kenneth Kaunda akiwa ameshika funguo za gari akisema kuwa, endapo wataifunga Tanzania, kila mchezaji atapewa gari na nyumba.
Joel Bendera alikuwa ndio kocha msaidizi, alipatwa na hasira na kuwaambia wachezaji kuwa “ Nyinyi hamjaahidiwa chochote, lakini nyinyi ndio mnatakiwa kutoa ahadi kwa Watanzania” , lakini kingine alichosisitiza Bendera , ni kuwa wasikubali kuwa mgongo wa watu wengine kupewa gari na nyumba.
Mpaka mapumziko Stars ashakula 1-0 , kwa mujibu wa Peter Tino aliyefanya mahojiano na gazeti la Mwananchi siku za nyuma, anasema uwanjani kulikuwa na watanzania 30 au 40 tu wakiwashangilia.
Wakati wa mapumziko baada ya kocha mkuu Mpoland Slowmir Wolk kumaliza kuongea na wachezaji, Bendera akapewa nafasi ya kuzungumza, hakuwa na mengi ya kusema, alirudia maneno yake yale yale “tusikubali watu wapewe nyumba na gari kwa mgongo wetu”
.
Zikiwa zimebaki dakika tano mchezo kumalizika mjini Ndola, mbele ya Rais wao Kenneth Kaunda, Peter Tino anaandika goli la kusawazisha, mechi inaisha, Tanzania inafuzu AFCON. Nahodha Leodgar Chilla Tenga na wenzake wanashangilia pamoja na shujaa wao Joel Bendera.
Agosti 26,1979 wakina Tenga hawakuahidiwa chochote, lakini Machi 24,2019 wakina Samatta wameahidiwa, wameahidiwa Shangwe na watanzania . Ndola watanzania hawakuzidi 40, kesho Machi 24 watanzania zaidi ya 60,000 watakuwepo uwanja wa Taifa.
Lakini licha ya kuahidiwa na watanzania, Samatta na wenzake wanatakiwa kufuata maneno ya Bendera, wanatakiwa kutoa ahadi kwa watanzania,ahadi yao ni moja tu, ushindi dhidi ya Waganda.
Achilia mbali matokeo ya Cape Verde na Lesotho, wachezaji wa Stars wanatakiwa kufanya kazi yao, “ Do your part and Relax”.
.
Joel Bendera ametangulia mbele za haki, lakini angekuwepo na kupewa nafasi ya kuongea na wachezaji wa Stars leo, angewaambia kuwa wanatakiwa kutoa ahadi kwa watanzania, na si nyingine, ni ushindi.
Shujaa wa mwaka 1979 kule Ndola ni Joel Bendera, lakini shujaa wa kesho pale Temeke ni wingi wa mashabiki wa Tanzania ambao uwepo wao utarahisisha ushindi kwa Taifa Stars.