Miili na Mioyo ya Watanzania haitakiwi kukaa sehemu moja Jumapili
Clatous Chota Chama pengine ni mtu anayechukiwa zaidi kwa sasa nchini Algeria kuliko nchini Congo na kwa mashabiki wa Yanga. Huyu ni shujaaa wa Simba lakini ni adui mkubwa kwa mashabiki wa JS Saoura ya nchini Algeria.
Jumamosi iliyopita mashabiki wa Algeria walikuwa wakifatilia zaidi mechi ya Simba na AS Vita kuliko mechi yao dhidi Al Ahly, mechi yao hawaikujali sana maana haikuwa inawahusu sana kama ile ya Simba na Vita. Mioyo yao ilikuwa Dar es salaam na miili yao ilibaki Alexandria, unajua ni kwa nini, ni kwa sababu pumzi ya uhai wao wa kubaki katika michuano ya klabu bingwa Afrika ilikuwa ipo Wilaya ya Temeke Dar es salaam, haikuwa Alexandria.
JS Sauora walihitaji sare tu kutoka katika mechi ya Simba na Vita ili wao wafuzu katika robo fainali licha ya kuwa walishafungwa na Al Ahly. Katika dakika ya 90 Mzambia Clatous Chama aliamua kuchukua pumzi yao ya uhai na kuipuliza kwa Simba, Mnyama akafuzu hatua ya robo fainali. JS Sauora hawakuwa na lakufanya tena, mioyo yao ikajaa chuki dhidi ya Mzambia huyo kama ilivyokuwa kwa Nkana, hivyo wakatolewa nje ya mashindano.
Machi 24 miili ya Watanzania inatakiwa iwepo Tanzania lakini mioyo yao inatakiwa kusafiri mpaka katika mji wa Praia nchini Cape Verde kwenye mchezo wa Cape Verde na Lesotho. Licha ya kuwa Tanzania wanataka ushindi dhidi ya Uganda, lakini ushindi huo utakuwa sawa na kuwa na bunduki ya AK-47 vitani ikiwa haina risasi kama Lesotho itashinda mechi yake na Cape Verde. Utabaki na sifa tu kuwa nina bunduki kubwa lakini haifanyi kazi, utakuwa nayo kama mzigo na vita utapoteza.
Ushindi wa Tanzania jumapili utakiwa na tija kama Lesotho hatapata matokeo ya ushindi dhidi ya Cape Verde, adui mkubwa wa ushindi huo ni Lesotho tu. Licha ya promotion kubwa ambayo inaendelea kufanywa kuelekea mechi hiyo, akili za Watanzania zinatakiwa kujua jumapili adui wao mkubwa si watoto wa Idd Amini, ni Lesotho.
Jumapili ya Machi 24, inaweza kuwa ni moja ya siku ya furaha katika historia ya soka Tanzania tangu mwaka 1980, na pia inaweza kuwa siku iliyojaa na huzuni endapo Lesotho watashinda mechi yao.
Sir Alex Ferguson mwaka 2012 yaliwahi kumtokea mambo kama haya, alishinda mechi yake dhidi ya Sunderland, huku akisubiri matokeo ya Man City na QPR ili kujihakikishia ubingwa wa ligi kuu, lakini Sergio Kun Aguero alifanya kama Chama alivyochukua pumzi ya JS Saoura, na kupeleka ubingwa kwa Sheikh Mansour.
Tanzania na Lesotho wote wana pointi 5 katika msimamo wa kundi L mpaka sasa, lakini Lesotho wapo nafasi ya pili na Tanzania ya tatu kwa sababu katika mechi mbili kati ya Tanzania na Lesotho, Lesotho waliondoka na pointi 4 huku Tanzania wakiondoka na pointi 1. Hivyo Tanzania ikishinda jumapili na Lesotho nae akashinda pia, ni Lesotho ndio wataenda AFCON, si Tanzania, wazungu wanaita “The hurtful truth” yaani ukweli unaouma.
Kwa msisitizo mkubwa tena, miili ya watanzania inatakiwa kuwa Tanzania huku mioyo yao iwe zaidi Praia,Cape Verde
Tusubiri tuone sinema hii ya kusisimua ambayo Watanzania wameisubiri kwa miongo karibia minne. Cha muhimu wakati watanzania wanaitizama Sinema hii siku ya jumapili, akili zao zijue kuwa inaweza kuisha kwa furaha au huzuni kubwa.B