Ally Bushiri afutwa kazi Mbao FC
Klabu ya Mbao FC ya jijini Mwanza imeripotiwa kuwa imefanya tena maamuzi mazito kuhusu kikosi chao kukumbwa na mwenendo usiofurahisha kiasi cha kuamua kumuondoa kocha wao aliyekuwa kadumu na klabu hiyo kwa muda mchache tu toka ateuliwe.
Mbao FC jana Machi 18 imetangaza kuachana na aliyekuwa kocha wake mkuu Ally Bushiri kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha timu yao, Mbao FC inafikia maamuzi hayo baada ya kudumu na kocha huyo kwa miezi minne pekee toka atangazwe kuwa kocha wa timu hiyo Desemba 19 2018 na kumrithi Amri Said aliyeachana na timu baada ya kuletewa Ally Bushiri kama msaidizi wake.
Kocha Ally Bushiri anafungashiwa virago vyake na uongozi wa Mbao FC akiwa anaiacha timu hiyo ikiwa nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2018/2019 wakiwa na alama 36 sawa na Stand United waliopo nafasi ya 16 ila wametofautiana magoli ya kufunga na kufungwa.
Wakati Amri Said anaondoka Mbao FC Desemba 19 2018 alikuwa kaifundisha timu hiyo katika michezo 17 ya Ligi, alishinda michezo 6, alifungwa michezo 5 na sare michezo 6, alifunga mabao 12 na kufungwa mabao 16 , awali timu hiyo ilikuwa nafasi ya 4 kwa kuwa na alama 24, hivyo chini ya Bushiri timu hiyo imevuna alama 12 katika michezo 13.