Zizou amvuta Sadio Mane Bernabeu
Zikiwa zimepita siku nane tu tokea klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania itangaze kwa kumrudisha aliyekuwa kocha wake Zinedine Zidane na kumfuta kazi Santiago Solari, Zidane ameonekana kuanza cheche za kujenga upya kikosi chake cha Real Madrid.
Zidane ambaye aliondoka Real Madrid miezi tisa iliyopita kufuatia ushindi wa mara tatu mfululizo wa Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya, imeripotiwa kuwa ameanza kutuma ofa za wachezaji anao wahitaji katika kikosi chake kipindi cha usajili cha dirisha kubwa.
Hii ni kwa mujibu wa mtandao France Football ambao ni moja kati ya vyanzo vya kuaminika vya habari za soka duniani kote, Zidane anataka kumsajili Sadio Mane kutokea klabu ya Liverpool, mtandao huo umetaja kuwa miongoni mwa wachezaji wachache wanaopewa kipaumbele ni pamoja na msenegal huyo.
Sadio Mane hadi leo Machi 19 akiwa na Liverpool amefunga magoli 11 katika mechi 11 zilizopita, akiwa na wastani kufunga bao moja kila mechi.
Mane sasa amefikisha jumla ya mabao 17 katika EPL akiwa nyuma ya Sergio Aguero anayeongoza kwa mabao 18, magoli yake 17 pia yamemfanya avunje rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kisenegal kufunga magoli mengi EPL (17) kwa msimu mmoja baada ya kuvunja rekodi iliyokuwa inashikiliwa na msenegal mwenzake Demba Ba aliyoiweka msimu wa 2011/2012 akiwa na Newcastle United na kufunga mabao 16.