Mbappe apigwa faini na PSG
Mtandao wa AS wa nchini Hispania umeripoti kuwa uongozi wa klabu ya Paris Saint Germain ya nchini Ufaransa umefikia hatua ya kuwapiga faini nyota wake wawili Kyliane Mbappe na Adrien Rabiot kutoka na kosa lao walilolifanya la kuchelewa wakati wa kikao cha wachezaji wa timu hiyo kuelekea mechi yao dhidi ya Marseille iliyopigwa jana.
Uongozi wa PSG umeamua kuwapiga faini wachezaji hao wa euro 180,000 (Tsh milioni 479) kila mmoja kutokana na kosa hilo, hiyo ni muendelezo wa kulinda na kujenga timu yao imara lakini iliyotawaliwa na wachezaji wenye nidhamu, kiasi hicho cha pesa walichopigwa faini kitapelekwa katika Foundation ya PSG.
Wote wawili kwa pamoja Kyliane Mbappe na Adrien Rabiot wamekiri kutenda kosa hilo na kusaini nyaraka maalum kama ilivyo kwa utaratibu wa PSG, huu umekuwa ni utaratibu wa kawaida kwa vilabu mbalimbali barani Ulaya kuwakata mishahara wachezaji wake au kuwapiga faini kwa makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu ikiwemo kuchelewa mazoezi au shughuli zozote za kitimu.