NDOTO YA NEYMAR KUCHEZA REAL MADRID INAZIDI KUFIFIA
Ni siku chache zimepita toka klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania itangaze kuwa imeamua kumrudisha aliyekuwa kocha wake wa zamani Zinedine Zidane aje aokoe jahazi baada ya klabu hiyo kuyumba kwa kiasi kikubwa msimu huu na kutokuwa na uhakika wa taji lolote.
Baada ya Zidane kutangazwa kuwa amerudi Real Madrid kwa mkataba wa miaka mitatu, mtandao wa AS umeripoti kuwa ndoto ya Neymar kwenda kucheza Real Madrid imefifia kutokana na Zidane kuushawishi zaidi uongozi wa Real Madrid umsajili Kyliane Mbappe na sio Neymar.
Ilikuwa inaaminika kuwa Neymar baada ya kwenda kucheza PSG na kudaiwa kuwa kapoteza nafasi ya kuja kushinda tuzo ya mchezaji bora wa dunia na mataji makubwa kama ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, anataka kuondoka PSG na kurudi Hispania na kuendeleza ndoto zake huku Real Madrid ndio ikitajwa kama chaguo lake sahihi, kwani kwa namna alivyoondoka Barcelona wengi hawaamini kama atahitajika tena.
Aidha mtandao wa AS umeeleza kuwa ujio wa Neymar Real Madrid utamlazimu Zidane kubadili kwa kiasi kikubwa mfumo wake, hivyo kwa sasa na asili ya mfumo anaotaka kuutumia chaguo lake la kwanza itakuwa ni Mbappe na sio Neymar ambaye amewahi kucheza Ligi Kuu Hispania kwa miaka minne (2013-2017).
Zidane hivi karibuni alinukuliwa akisema kuwa “Nawapenda wachezaji wote wazuri lakini ningependa kumfundisha Kylian Mbappe”