Dembele ni bora kuliko Neymar
Moja kati ya habari ambayo iliwahi kuwaumiza mashabiki wa timu ya FC Barcelona na uongozi wao ni taarifa za aliyekuwa mshambuliaji wao Neymar kulazimisha uhamisho wa kuondoka FC Barcelona na kujiunga na timu ya Paris Saint Germain ya nchini Ufaransa.
Baada ya matakwa ya Neymar kutimia ya kuihama klabu hiyo kwa kile kilichodaiwa na wengi kuwa anafichwa na Messi kama staa wa timu, Rais wa FC Barcelona na uongozi wake walimsajili Ousmane Dembele kutoka Borussia Dortmund kama mbadala wa Neymar.
Licha ya Neymar kuwa na jina kubwa na kuaminika kuwa na uwezo mkubwa Rais wa Barcelona Josep Maria Bartomeu amesema kuwa kwake Dembele ni bora kuliko Neymar, kauli ambayo aliitoa katika kituo cha radio nchini Hispania Cadena SER alipoulizwa kuwa wana mpango wa kumrudisha Neymar kama inavyodaiwa?
.
“Dembele ni bora kuliko Neymar. Kuhusu kumrudisha tena (Neymar) siwezi kusema ndio au hapana, ila Barcelona ilicheza kamari mara ya kwanza kumuuza Neymar na kutumia zile pesa kumsajili mchezaji kama Dembele na Coutinho, (Dembele) yupo Barca kwa sasa na yeye ni bora kuliko Neymar” alisema Josep Maria Bartomeu
Neymar wakati anaondoka Barcelona na kwenda kujiunga na Paris Saint Germain 2017, aliuzwa kwa pauni milioni 199 na ndio pesa hizo Barcelona wakazitumia kufanya usajili wa wachezaji kama Coutinho na Dembele.