Suarez ashindwa kuficha furaha kuhusu Madrid kutolewa ligi ya Mabingwa
Sasa ni wazi utamaduni wa mashabiki wa timu za taifa moja kushangilia timu za kigeni zinapokuja kucheza na wapinzani wao katika nchi husika, watapata mashabiki kutoka upande wa pili wa wapinzani wao wakipenda timu hiyo ifungwe kwa sababu tu ni wapinzani wao wa jadi.
Tanzania Simba inapocheza na timu ya kigeni Yanga huishangilia timu hiyo ya kigeni, Misri Al Ahly inapocheza na timu ya kigeni mashabiki wa wapinzani wao Zamalek wataishangilia timu ya kigeni ,ndivyo hivyo ilivyo nchini Hispania kwa mashabiki wa FC Barcelona walikuwa wakiishangalia Ajax katika mchezo dhidi ya Real Madrid.
Hilo limedhihirika baada ya nyota mpya wa FC Barcelona Fank De Jong aliyepo kwa mkopo Ajax, kuweka wazi kuwa wakati anasaini mkataba wa kuichezea FC Barcelona hivi karibuni aliambiwa kuwa ahakikishe kuwa anaitoa Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kama walivyofanya kwa kuifunga 4-1 (agg 5-3) na kuitoa kwenye hatua ya 16 Bora.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay ambaye pia anaichezea FC Barcelona Luis Suarez ameweka wazi msimamo wake kuwa nae alikuwa anaishangilia Ajax katika mchezo dhidi ya Real Madrid wa Ligi ya Mabingwa Ulaya “Hongereni ,siku zote nimekuwa shabiki wa Ajax” Suarez aliandika kupitia twitter yake pamoja na kusema kuwa amekuwa shabiki wa Ajax muda mrefu lakini hakuwahi kupost kabla ya hapo.
Hata hivyo Mruguay huyo amewahi kuichezea Ajax kati ya mwaka 2007 na 2011.