Dismas Ten ajibu kuhusu Ndemla kwenda Yanga
Kwa zaidi ya wiki sasa kuwa kama kuna maneno ya chini kwa chini kupitia mtandao wa kijamii wa instagram kutoka kwa afisa habari wa Simba Haji Manara kwenda kwa afisa habari wa Yanga Dismas Ten kuhusiana na kiungo wa timu ya Simba SC Said Ndemla.
Dismas Ten amekuwa akipost picha za Ndemla kwa masihara kama kasajiliwa na Yanga kimya kimya vile, huku Haji Manara nae akijibu kwa vijembe na kusema wana Simba wapuuze hizo taarifa mchezaji huyo ni mali yao wala wasitishike.
Azam TV baada ya droo ya kupanga mechi za robo fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup, waliongea na afisa habari wa Yanga Dismas Ten na kutaka afafanue kuhusiana na jambo hilo na vipi Said Ndemla ni kweli anaenda Jangwani au?
“Ndemla ni mchezaji mzuri hakuna ambaye hafahamu juu ya Said Ndemla, mtu yoyote ukimuuliza kuhusu wachezaji wa Tanzania wenye vipaji hawezi kuacha kumtaja Said Ndemla, Ndemla mimi ni rafiki yangu kuhusu kusajiliwa Yanga au kuto kusajiliwa hilo ni suala linalohusu kamati yetu ya usajili na benchi la ufundi ,yote yanaweza kusemwa mwisho wa msimu lakini kwa sasa hivi huwezi kusema lolote” alisema Dismas Ten kupitia Azam TV