Hii ndio sababu ya Solskjaer kuvaa bib jana
Pengine wewe ni moja ya watu ambao tulijiuliza kwa nini kocha wa Man United Ole Gunnar Solskjaer alivaa bibs ya njano jana kwenye mchezo dhidi ya PSG na hatukupata jibu kwa muda ule ambao mechi inaendelea.
Mwanzoni mwa mchezo Solskjaer aliingia akiwa amevaa nguo nyeusi kutoka juu mpaka chini, lakini baada ya muda mchache tulishuhudia amevaa bib ya njano,ambapo ikazua utani mitandaoni kuwa huenda kocha huyo amejiweka kwenye orodha ya wachezaji watakaoingia kama sub ili kupindua matokeo kama alivyofanya 1999 Camp Nou.
Imethibitishwa kuwa kocha huyo aliambiwa na mwamuzi wa akiba avae bibs ya njano kwa sababu alikuwa amevaa nguo nyeusi na wachezaji wa PSG nao walikuwa wamevaa jezi za rangi nyeusi, hivyo kwa upande ambao Solskjaer alikuwa anatembea kwenye touchline alikuwa anamchanganya mshika bendera ambaye alikuwa kwenye upande mwingine wa uwanja kufanya maamuzi, hasa maamuzi ya offside, hivyo mshika kibendera alikuwa anamchanganya na wachezaji wa PSG kutokana na rangi zao kufanana.
Kwa upande wa kocha wa PSG Thomas Tuchel nae alikuwa amevalia nguo nyeusi kama Ole, lakini yeye alibaki vile vile bila kuvaa kingine kwa sababu upande ambao alikuwepo kwenye touchline, ndio upande huo huo mshika kibendera mwingine alikuwepo, hivyo hakukuwa na mkanganyiko wowote.