Romelu Lukaku akataa kuhusu kugombana na Pogba
Mshambuliaji wa Man United Romelu Lukaku amekanusha taarifa zinazosambaa zikisema kuwa aligombana na mchezaji mwenzake Paul Pogba kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Southampton Jumamosi iliyopita.
Mitandao kadhaa barani Ulaya iliripoti Lukaku aligombana na Pogba kwa sababu ya kumnyima nafasi ya kupiga penati ili aweze kuondoka na Hat Trick kwenye mechi hiyo ambapo alifunga goli mbili.
Ripoti hizo zilisema kuwa Lukaku alimkumbusha Pogba jinsi alivyokuwa akimsaidia kipindi kile akiwa hawaelewani na kocha Jose Mourinho.
Wakati penati hiyo inapatikana ilikuwa ni dakika za mwisho, Man United wakiongoza 3-2,huku Romelu Lukaku akiwa amefunga goli mbili, Pogba ambaye ndiye mpigaji wa penati alipiga na kukosa.
Taarifa zilieleza kuwa Lukaku alimwambia Pogba kuwa angekuwa kwenye nafasi yake, angetoa hiyo penati na kumpa mfano wa Mo Salah alivyompa penati Roberto Firmino kwenye ushindi wa 5-1 dhidi ya Arsenal Disemba mwaka jana ili aweze kukamilisha Hat-Trick yake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo Pogba alimjibu Lukaku kuwa, kama mpigaji wa penati wa siku zote alikuwa na haki zote za kupiga.
Kocha Ole Gunnar Solskjaer ndiye aliyeripotiwa kuamualia ugomvi huo na kuwaambia hawatakiwi kugombana ndani au nje ya uwanja.

Romelu Lukaku leo kupitia mtandao wa Twitter ameamua kuvunja ukimya na kusafisha hali ya hewa kwa kuthibitisha taarifa hizo si za kweli, “Chuki inaposhindwa kufanya kazi,wanaanza kuongea uongo” aliandika Lukaku kwenye akaunti yake ya Twitter.