Uganda waanza kuandaa silaha za kuiua Tanzania
Pamoja na kuwa timu ya taifa ya Uganda The Cranes imeshakata tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika 2019 nchini Misri, ila imeonekana kuwa wanajiandaa kwa umakini mkubwa kuelekea kucheza mchezo wao wa mwisho wa Kundi L wa kukamilisha ratiba ya Kundi L ya michezo ya mwisho.
Uganda watacheza dhidi ya Tanzania katika uga wa uwanja wa Taifa Machi 24 lakini ikiwa bado wiki kadhaa kocha wa timu hiyo Sebastien Desabre ametaja majina ya wachezaji 46 kueleka mchezo huo dhidi ya Tanzania wakiwa tayari wamefuzu.
Uganda wameita wachezaji 31 wanaocheza Ligi ya ndani ya Uganda na watachuja na kusalia tisa ambao wataungana na wachezaji wengine 15 wanaocheza nje ya Ligi ya Uganda wakiwemo Emmanuel Okwin na Juuko Murshid wa Simba, hivyo watakuwa jumla ya wachezaji 24 watakaoweka kambi ya Cairo Misri ya siku nne kuanzia Machi 18 hadi 22 na baadae kuanza safari ya Tanzania.
Tanzania wapo Kundi L lenye timu za Uganda ambaye tayari amefuzu, Cape Verde na Lesotho timu ambazo zote zina nafasi hivyo mchezo wao wa mwisho ni muhimu sana kwa kila timu, Uganda wanaongoza kwa alama 13, wakifuatiwa na Lesotho walio na alama 5 sawa na Tanzania walipo nafasi ya tatu na Cape Verde anashika mkia kwa kuwa na alama 4.