Baada ya miaka 10 Valencia kuondoka Man United
Kocha wa muda wa Man United Ole Gunnar Solksjaer amefungua mlango wa kuondoka kwa nahodha Antonio Valencia ambaye amekuwa ni mtumishi wa timu hiyo kwa miaka 10.
Valencia amecheza mechi nane tu msimu huu na mechi ya mwisho kucheza ni Januari 2.
Man United wanahitajika kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja kabla ya saa 11 jioni leo ijumaa , na isipokuwa hivyo mchezaji huyo ataondoka huru majira ya kiangazi.
Lakini kwa mujibu wa Solskjaer leo, amesema kuwa hadhanii kama ataongezewa mkataba, na hivyo ni wazi kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ecuador ataondoka mwisho wa msimu.
“Amekuwa na maisha mazuri hapa Manchester na England, na ni mmoja wa washindi wa ubingwa wa ligi kuu waliobaki katika vyumba vya kubadilishia nguo, lakini sina uhakika Man United na Antonio watakubaliana kuendelea mpaka mwakani” amesema Solskjaer.
Akiwa na Man United amechukua ubingwa wa ligi kuu mara mbili, kombe la FA mara moja,kombe la ligi mara mbili,Europa League mara moja na ngao ya jamii mara moja.