Romelu Lukaku ataka kucheza na Ronaldo
Nyota wa kimataifa wa Ubelgiji anayekipiga katika klabu ya Manchester United ya nchini England Romelu Lukaku ameripotiwa na mitandao mikubwa ya habari ikiwemo mtandao wa beiNSports kuwa yupo radhi kujiunga na Juventus kama klabu yake ya Manchester United haitokuwa na mpango nae mwisho wa msimu.
Mtandao wa The Sun pia unaeleza kuwa kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya uongozi wa Manchester United watakuwa radhi kusikiliza ofa za kumuuza Romelu Lukaku mwisho wa msimu, kitu ambacho kinaelezwa kuwa kimemfikia Lukaku na kwa upande wake anatamani kucheza nje ya England na chaguo lake la kwanza ni kwenda kucheza Juventus.
Pamoja na kuwa Lukaku amekuwa na hamu ya kwenda kucheza Juventus ambapo atapata fursa ya kucheza na nyota wa zamani wa Manchester United Cristiano Ronaldo, haijafahamika kama Juventus watahitaji huduma ya Lukaku na kutuma ofa Old Trafford au la.
Lukaku alisajiliwa Manchester United akitokea Everton 2017 chini ya utawala wa Jose Mourinho lakini katika kipindi chote hicho akiwa na Manchester United katika Ligi Kuu ya England amefunga jumla ya mabao 26 katika michezo 59 na kati ya hiyo michezo 10 hakucheza kwa dakika zote 90.