Sarri na Arrizabalaga wasafisha hali ya hewa
Kocha wa klabu ya Chelsea Maurizio Sarri amewashangaza baadhi ya waandishi wa habari baada ya kuulizwa kuhusiana na mabadiliko aliyoyataka kuyafanya dakika ya 119 wakati wa mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi kati ya Chelsea dhidi ya Manchester City akitaka kumtoa mlinda mlango Kepa Arrizabalaga aliyegoma kumpisha Caballero.
Sarri baada ya Kepa Arrizabalaga kugoma kutoka ilibidi mchezo uendelee na alionesha hasira kwa kitendo cha Kepa lakini alipoulizwa na waandishi wa habari alisema alihisi Kepa kaumia ndio maana akataka kufanya mabadiliko lakini alisema anaweza kuendelea kucheza kama kawaida.
.
“Nafikiri tunatakiwa kuzungumzia mpira kwa hapa kwa sababu tulicheza mchezo mzuri sana, katika ile hali hatukuwa tumeelewana tu , nilihisi golikipa ameshikwa na misuli na asingeweza kuendelea na mikwaju ya penati kumbe tatizo haikuwa misuli na angeweza kuendelea kucheza hatua ya penati,lakini nililijua hilo baada ya dokta kurejea benchi” alisema Sarri aliyekiri kuwa atamuita kipa huyo kumuelekeza namna ya kujibu.

Kwa upande wa Arrizabalaga amesema kuwa anaelewa kinachoendelea kuongelewa kwenye televisheni na mitandao ya kijamii kuhusiana na kitendo hicho, na kusisitiza kuwa halikuwa lengo lake kupingana na kocha wake bali ni kutokuelewana kwa wakati ule ndio kulisababisha hilo, kocha akifikiri amepata maumivu wakati yeye ni mzima.
“ Nilikuwa ninajaribu kumwambia niko sawa. Alikuwa anafikiria sipo sawa “
.
“ Zilikuwa dakika mbili au tatu za mkanganyiko mpaka madaktari walivyorudi kwenye benchi na kuelezea kila kitu vizuri “
Pamoja na hayo mchezo huo wa fainali uliyomalizika dakika 120 pasipo kufungana, ulimalizwa kwa hatua ya mikwaju ya penati iliyoipa Manchester City Ubingwa kwa penati 4-3 huku Kepa Arrizabalaga aliyegoma kufanyiwa mabadiliko ya kumpisha Caballero akicheza penati moja pekee.
