Cantona ampa sifa Solskjaer kwa kumbadili Pogba
Miongoni mwa vitu ambavyo vimekuwa vikimuweka katika vichwa vya habari kiungo wa kimataifa wa Ufaransa na Manchester United Paul Pogba ni pamoja na muonekano wake wa nywele, Pogba amekuwa ni miongoni mwa wachezaji wanaopenda kubadilisha mitindo ya nywele kila kukicha ,kiasi cha kufikia kukosolewa na baadhi ya watu pale anapokuwa amecheza vibaya huku akiwa na mtindo mpya wa nywele.
Pogba chini ya kocha wa zamani wa Manchester United Jose Mourinho aliwahi kubadili mitindo ya nywele mara kwa mara, kitu ambacho kilimfanya asakamwe sana na watu mitandaoni ukizingatia timu yao ilikuwa haipati matokeo mazuri.
Mkongwe wa zamani wa klabu ya Manchester United Eric Cantona ametoa kauli inayoashiria kuwa kwa sasa kocha wa muda wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer ameibadilisha timu hiyo kuanzia wachezaji, hadi mfumo mzima wa uchezaji ikiwemo kwa kiungo wao Paul Pogba ambaye alikuwa na matatizo na kocha Jose Mourinho aliyefutwa kazi Desemba.

Cantona ambaye ana umri wa miaka 52 kwa sasa alicheza Manchester United kwa miaka mitano pekee (1992-1997), amesema kuwa tangu Solskjaer atue Machester United Paul Pogba hajabadili mtindo wa nywele “Toka Ole Gunnar Solskjaer ametua Manchester United Paul Pogba hajabadili mtindo wa nywele, labda amemwambia kuwa kipaumbele chake ni kucheza mpira na sio kingine”