Marc Bartra aeleza Xavi alivyomsaidia Barca
Mlinzi wa kati wa zamani wa FC Barcelona ya nchini Hispania anayeitumikia Real Betis kwa sasa Marc Bartra amekiri kuwa moja kati ya vitu vilivyomjenga katika soka lake ni pamoja na maneno ya hekima ya mkongwe wa Barcelona wakati huo Xavi Hernandez.
Marc Batra ambaye ana umri wa miaka 28 kwa sasa ni zao la kituo cha FC Barcelona cha kukuzia vipaji kinachojulikana kwa jina la La Masia na mara yake ya kwanza kucheza timu ya wakubwa ya FC Barcelona ilikuwa mwaka 2010 akiwa na umri wa miaka 19.
Ila wakati anaingia uwanjani Xavi wakati huo akiwa anaitumikia timu hiyo alimtolea kauli ambayo ilimuondoa hofu na kumfanya acheze kwa kujiamini ukizingatia ametokea timu za vijana , Xavi alimwambia Bartra kuwa “Tulia na mpira kama hujui wapi pakuupeleka ukiupata nipasie mimi na kama kuna mpinzani nyuma yako nipasie pia mimi” Bartra alisema hayo wakati akihojiwa na L’Equipe.
Tukukumbushe tu Marc Bartra aliichezea FC Barcelona akitokea timu ya vijana kwa miaka sita (2010-2016) na kuichezea michezo 59 na kufunga mabao matano kabla ya kujiunga na Borussia Dortmund ya Ujerumani (2016) kwa ada ya uhamisho wa euro Milioni 8, alikocheza mechi 31 kabla ya Januari 2018 kurudi Hispania katika klabu ya Real Betis.