Huu ni msiba mzito kwa Chelsea
Klabu ya Chelsea imefungiwa na FIFA kufanya usajili katika madirisha mawili yajayo kwa kosa la kuvunja sheria za usajili kwa wachezaji wa kigeni walio chini ya umri wa miaka 18.
Adhabu hiyo ina maana kuwa Chelsea hawataweza kufanya usajili katika dirisha la usajili la kiangazi mwaka huu na pia dirisha la mwezi Januari.
Pia The Blues wamepigwa faini ya pauni 460,000 kwa makosa hayo na chama cha soka cha England FA na wamepigwa faini ya pauni 390,000 kwa kuvunja sheria kwa kuhusika katika kuunganisha usajili huo.
Klabu hiyo imekutwa na hatia ya matukio 29 ya kuvunja ibara ya 19, ambayo inahusiana na usajili wa wachezaji chini ya miaka 18.
Moja ya kesi ambayo ilikuwa inafanyiwa uchunguzi na FIFA ni kiungo wa kimataifa wa Burkina Faso Bertrand Traore ambaye mwaka 2017 aliuzwa na Chelsea kwenda Lyon kwa pauni milioni 8.8 huku kukiwa na kipengele cha kumnunua tena endapo wakimhitaji.
Madai yaliyoripotiwa ni kuwa Traore alisajiliwa na Chelsea akiwa ni mwanafunzi wa shule akiwa na miaka 16, ingawa Chelsea walikataa mchezaji huyo kuwepo kwa vitabu vyao.
Hata hivyo Chelsea wanayo nafasi ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo ambayo itawafanya wasisajili mchezaji mpaka majira ya kiangazi mwaka 2020.