Kisa cha kuhuzunisha kwa timu ya Italia iliyopigwa 20-0
Rais wa chama cha mpira wa miguu nchini Italia Gabriele Gravina ameeleza kuwa kipigo cha mabao 20-0 cha Pro Piacenza kutoka kwa Cuneo katika mchezo wa Ligi daraja la tatu nchini Italia maarufu kwa Serie C ni udhalilishaji katika michezo.
Kabla ya mechi hiyo ya jumapili iliyopita Pro Piacenza ambayo ipo kwenye ukata kiuchumi walishindwa kucheza mechi tatu mfululizo za ligi hiyo, ambapo wapinzani wao Pro Vercelli, Juventus II na Siena walipewa ushindi wa 3-0 kila mmoja.
Katika kuepusha kushushwa daraja kwa kukosa mechi nne mfululizo kutokana na wachezaji na benchi la ufundi kugoma kucheza, ilibidi timu hiyo kupeleka wachezaji wao wa kikosi cha vijana siku hiyo ya jumapili, ambapo walianza mechi hiyo wakiwa na wachezaji 7 kutokana na sheria zao zinaruhusu mchezo kuanza timu ikiwa na wachezaji sita uwanjani.
Wachezaji hao wote saba umri wao ulikuwa kati ya miaka 16 na 19. Nahodha wao Nicola Cirigliano mwenye umri wa miaka 18 ndiye aliyekuwa kocha wao.
Mpaka mapumziko,Piacenza walikuwa wamepigwa goli 16-0 na kipindi cha pili wakaongezwa magoli manne na mchezo kuisha kwa kupokea kipigo cha goli 20-0.
Pro Piacenza walikuja uwanjani wakiwa wachezaji nane lakini walianza saba kutokana na mchezaji wao mmoja kusahau kitambulisho.
Hawakuwa na mchezaji wa akiba, hivyo baadae ilibidi daktari wao wa viungo vya mwili mwenye umri wa miaka 39 aingie kama sub.
Jumatatu hii timu uongozi wa Serie C ulitangaza kuitoa timu hiyo kwenye mashindano kutokana na kukiuka sheria za ligi kama vile kuchezesha wachezaji ambao hawana usajili wa kucheza katika ligi hiyo.