Singida na Ndanda kukipiga Dar
Kutokana na Ugumu wa ratiba ya Ligi na kombe la FA, Mchezo wa FA kati ya Singida United na Coastal Union utachezwa Dar es Salaaam tar 23/02/2019 badala ya Singida kama ulivyopangwa awali.
Ikumbukwe leo Jumatano (20/02/2019) Singida United inacheza dhidi ya Ndanda Fc huko Mtwara, hivyo kesho tar 21/02/2019 timu inatakiwa iondoke Mtwara kurejea Singida ambapo kwa umbali wa Mtwara hadi Singida ni safari ya Siku mbili, hivyo timu ingefika Singida tar 22/02/2019.
Wakati huo huo tar 23/02/2019 Klabu hiyo inatakiwa kucheza mechi ya kombe la FA hapa nyumbani Namfua.
Mkurugenzi mtendaji wa Singida United Festo Sanga amesema jambo hilo wameona sio salama kwa Afya ya wachezaji na mchezo husika.
“sisi viongozi wa Singida United tumeiomba TFF wanaosimamia kombe la Azam Sports Federation Cup (FA) watubadilishie Uwanja ili kuendana na muda, angalau timu ipumzike na iweze kucheza tar 23/02/2019.
Tunawashukuru TFF wamekubali ombi letu na wametupatia Uwanja wa Azam Complex saa 1:00 usiku siku ya tar 23/02/2019 ndipo mchezo wetu utakapofanyika dhidi ya Coastal Union.
Tunaomba radhi kwa mashabiki na wanasingida, tumefanya hivi kwa afya ya wachezaji wetu na mchezo wenyewe” amesema Sanga