Kutoka kwa Wayne Bridge na Terry mpaka Yondani na Ajib
Februari 2010 beki wa kushoto Wayne Bridge akiwa Man City alikataa kumpa mkono beki wa Chelsea John Terry katika mechi iliyokutanisha timu zao, sababu ya Bridge kukataa kumpa mkono Terry ni kufuatia nahodha huyo wa Chelsea kutoka kimapenzi na aliyekuwa mpenzi wake Vanessa Perrencel, ambaye nae alikuwa ni rafiki wa karibu wa mke wa John Terry, Toni.
Baadae mwezi huo wa Februari Wayne Bridge aliamua kujitoa moja kwa moja katika timu ya taifa ya England kutokana na tukio hilo kusalitiwa na John Terry, ambaye alikuwa ni rafiki yake.
Februari 2019, ikiwa imepita miaka tisa tangu kutokea tukio hilo la Wayne Bridge na John Terry, nchini Tanzania katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam linatokea tukio kama hilo baina ya mchezaji Kelvin Yondani na Ibrahim Ajib, wote wakiwa wachezaji wa Yanga.
Je hawa nao sababu yao ni kama ya Bridge na Terry ??? Lahasha, sivyo , hawa sababu yao ni nyingine, haifanani na ya hao wengine.
Januari 4 2019 klabu ya Yanga kupitia kwa kocha wake mkuu raia wa Congo na Ufaransa Mwinyi Zahera alitangaza maamuzi mazito ya kumvua nafasi ya unahodha wa timu hiyo Kelvini Yondani na kumpa Ibrahim Ajib kwa madai ya kuwa Yondani ni mtovu wa nidhamu hivyo amepoteza sifa ya kuwa kiongozi wa timu.
Kilichopelekea hayo yote ni kitendo chake cha Yondani kuchelewa kufika mazoezini, baada ya wachezaji kupewa siku tano za mapumziko na yeye kuja siku inayofuatia bila kutoa taarifa kwa kiongozi yoyote.
Baada ya hilo kutokea wakati wa mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba jana Februari 16, kabla ya mchezo huo kuanza Ibrahim AJib akiwatambulisha wachezaji wenzake kwa mgeni rasmi, Yondani alikataa kupeana mkono na Ajib licha ya Ajib kunyoosha kwa muda mrefu, ndipo maneno yakazidi kuzuka kuwa inawezekana ni ishu ya beji ya unahodha ambayo kavuliwa yeye na kupewa Ajib.