Mnyama aunguruma tena Taifa,safari hii dhidi ya Yanga
Mtanange wa watani wa jadi umepigwa leo katika dimba la uwanja wa Taifa, mashabiki wa Simba wakifurika kwa wingi kuwashinda wapinzani wao Yanga .
Pengine ushindi dhidi ya Al Ahly katika mechi ya jumanne hii iliwapa kiburi zaidi mashabiki wa Simba na kuwafanya kutinga uwanjani bila uoga.
Wachezaji wa Simba SC hawakuwa nyuma kuwaongezea kiburi mashabiki wao, goli la Meddie Kagere dakika ya 71 lilitosha kuwapa Simba dhidi ya watani wao wa jadi ambao waliondoka uwanjani wakiwa kichwa chini.
Baada ya mechi kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amesema kuwa kikosi cha Simba kina wachezaji bora kuliko wao, huku akisisitiza kuwa timu yake hawakuwa makini katika eneo la ushambulizi.
Kwa upande wa Simba kocha wao Patrick Aussems amesema kuwa amefurahi timu yake kuibuka na ushindi huo, na kusifu uwezo walioonesha wachezaji wake.
Ushindi huu sasa unawafanya Simba kufikisha pointi 39 kwenye ligi kuu wakiwa wamecheza mechi 16 huku Yanga wakibaki na pointi zao 58 wakiwa wamecheza mechi 24.