Ramos hatiani kufungiwa Klabu Bingwa Ulaya
Beki wa Real Madrid Sergio Ramos amekataa tuhuma za kutafuta kadi ya njano kwa kusudi kwenye mchezo wa jana wa hatua ya 16 bora klabu bingwa Ulaya dhidi ya Ajax.
Njano hiyo aliyoipata dakika ya 89 ya mchezo huo ambao Real Madrid walishinda kwa goli 2-1, inamfanya kufikisha kadi tatu za njano kwenye michuano hiyo msimu huu hivyo itafanya akose mechi ya marudiano itakayochezwa Santiago Bernabeu na kurejea akiwa msafi katika hatua ya robo fainali ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na mpinzani mkali.
Watazamaji na wachambuzi wameeleza kuwa alifanya hivyo kwa makusudi kupata kadi hiyo, lakini mchezaji huyo baadae kupitia mtandao wa Twitter alisema kuwa hakuitaka kadi hiyo kwa makusudi kama wengi walivyosema.
Sheria za UEFA zinasema kuwa mchezaji atafungiwa mechi mbili au kwa kipindi fulani kitakachotajwa kama atagundulika amepata kadi ya njano au nyekundu kwa kukusudia.