Wachezaji wa Leicester City kufanya maamuzi kuhusu mechi ya Cardiff City.
Wachezaji wa Leicester City wapo katika mpango wa kuahirisha mchezo wao wa ligi wikiendi hii dhidi ya Cardiff City kutokana na kupata msiba wa kufiwa na mmiliki wao Vichai Srivaddhanaprabha.
Wachezaji hao jana walikuwa katika uwanja wa King Power wakitoa heshima kwa tajiri huyo ambaye amepoteza maisha kwa ajali ya Helikopta iliyotokea Jumamosi nje ya uwanja huo.
Mchezo wao wa Carabao Cup ulipangwa kupigwa leo Jumanne, lakini tayari umeshaahirishwa.
Maamuzi ya kuahirisha mchezo huo wa ugenini dhidi ya Cardiff bado hayajafanywa, lakini wachezaji wamepewa ruhusa tayari ya kufanya maamuzi.
Uongozi wa ligi kuu na Cardiff wanaelewa mguso walionao wachezaji hao Leicester City na wapo tayari kusikiliza maamuzi yao.
Wachezaji wengi walikuwa karibu na Srivaddhanaprabha na mchezaji kama Jamie Vardy alionekana mwenye huzuni kubwa wakati akitoa heshima zake hapo jana akiambatana na mtoto wa mmiliki huyo, Aiyawatt ambaye ni makamu mwenyekiti wa klabu.
Mazoezi ya Jumapili ya Leicester City yaliahirisha baada ya tukio hilo kutokea Jumamosi ambapo walifariki watu wote watano waliokuwemo kwenye Helikopta hiyo.
Kipa Kasper Schemeicher alikimbilia eneo la tukio muda mfupi tu baada ya ajali kutokea. Ni moja ya wachezaji ambao wanaonekana kutokuwa tayari kiakili kurudi uwanjani kucheza mechi kwa sasa.