Kocha wa Simba anaamini Al Ahly waliwachukulia poa
Simba SC ya Tanzania imeendeleza harakati zake za kurudisha heshima katika soka la Afrika Kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly walioupata leo uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam shukrani zikitajwa kwenda kwa Zana na John Bocco waliompikia bao safi Meddie Kagere dakika ya 65.
Baada ya mchezo huo Simba ambao wanataraji kwenda Algeria sasa kucheza dhidi ya JS Saoura Machi 9, kocha wao Patrick Aussems aliongea na waandishi wa habari na kueleza kuwa pamoja na kufungwa kwa mabao 5-0 katika michezo miwili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kabla ya hapo alieleza kuwa hawezi kupata matokeo katika michezo dhidi ya Al Ahly na AS Vita.
“Nilisema kabla ya michezo ya Congo na Misri tuliocheza dhidi ya AS Vita na Al Ahly sitegemei kupata alama yoyote lakini nilijua nyumbani wakati wowote tunaweza kupambana na timu yoyote Kubwa Afrika leo tumecheza mchezo kwa kiwango cha hali ya juu kukiwa na presha ya juu, sijui kama hii timu ilitudharau baada ya kutufunga 5-0 wakajua itakuwa ni mchezo rahisi kwao? lakini kama mlivyoona tumewaonesha kuwa sisi sio klabu ya kutoka vijijini” alisema kocha wa Simba Patrick Aussems baada ya mchezo mbele ya waandishi wa habari
Hata hivyo pamoja na hayo bado Kundi D lililo na timu za Simba ya Tanzania, Al Ahly ya Misri, AS Vita ya Congo na JS Saoura ya Algeria lipo wazi na na timu zote zinaweza kufuzu hatua ya nane bora, kwani JS Saoura baada ya kuifunga AS Vita 1-0 na Simba kuifunga Al Ahly 1-0, Kundi limezidi kuwa wazi.
Kundi D kwa sasa linaendelea kuongozwa na Al Ahly ambaye ana alama 7, akifuatiwa na Simba SC wenye alama 6, JS Saoura wenye alama 5 wakishika nafasi ya tatu wakati AS Vita ambao walikuwa wanapewa nafasi kuwa watafanya vizuri zaidi katika michuano hiyo wakishika mkia kwa kuwa na alama zao 4 na sasa Al Ahly pia atakuwa Kinshasa Machi 9 kucheza dhidi ya AS Vita.