Maneno ya Wenger kwa Solskjaer yatimia
Mapema kabla ya mchezo wa kwanza wa 16 bora wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Manchester United dhidi ya Paris Saint Germain katika dimba la Old Trafford kuanza, kocha wa zamani wa klabu ya Arsenal anayefahamika kwa jina la Arsene Wenger alimuonya kocha wa mpito wa Manchester United kuwa awe makini na PSG kwani takwimu wakati mwingine zinadanganya.
Wenger mwenye umri wa miaka 69 kwa sasa aliyasema maneno hayo huku akimtetea kocha wa zamani wa Manchester United aliyefutwa kazi hivi karibuni Jose Mourinho, ambaye kufukuzwa kwake kumekuwa kukihusishwa na kugombana kwake na Paul Pogba, Wenger alieleza na kufika mbali zaidi kuwa Ole Gunnar Solskjaer ambaye ana heshimu uwezo wake lakini ameanza vizuri katika kikosi hicho kutokana na kukutana na ratiba nyepesi katika michezo yake.
Kocha huyo wa zamani aliyedumu na Arsenal kwa takribani miaka 22 aliifananisha ratiba ya mechi ya Manchester United chini ya Ole Gunnar Solskjaer kama ni fungate tu lazima liwe na mwisho, huku akisema walichoshindwana Pogba na Mourinho ni nidhamu, Mourinho ni muumini wa mchezaji mwenye nidhamu wakati Paul Pogba alikuwa anakosa nidhamu kidogo ndio maana alikuwa hapati nafasi chini ya Mourinho ila anakiri kuwa Mourinho ni kocha bora.
“Mourinho amethibitisha kuwa yeye ni kocha wa kiwango cha juu lakini yeye siku zote ni muumini wa nidhamu kwa kila mmoja aliyekatika timu, Pogba ni kiungo mzuri lakini wakati mwingine anakosa nidhamu” alisema Wenger alipokuwa akihojiwa na bEIN Sports na kueleza zaidi kuwa Solskjaer ana vimelea vya kuwa na bahati na kutokana na ratiba yake ya mwanzo pia alicheza na timu kama Cardiff, Huddsfield, Bournemouth, Newcastle na Reading.
Maneno ya Wenger yametimia usiku wake kwa Manchester United kufungwa kwa mabao 2-0, kama alivyokuwa amesema mchana wake kuwa fungate yaani kupata ushindi mfululizo lina mwisho wake na ndicho kilichotokea na sasa ana mtihani wa kwenda ufaransa Machi 6 katika mchezo wa marudiano kubadili matokeo na kuitoa PSG.