PSG wapata pigo lingine kuelekea Old Trafford
Majonzi juu ya majonzi kwa klabu ya Paris Saint Germain ya nchini Ufaransa ikiwa inaelekea mchezo wake wa kwanza muhimu wa hatua ya 16 bora wa michuano ya klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Manchester United katika uwanja wa Old Trafford uliyopo katika jiji la Manchester nchini England siku ya Jumanne ya Februari 12.
PSG wamepata pigo jingine kufuatia kuumia mguu kwa mshambuliaji wao tegemeo Edinson Cavani zikiwa zimepita siku chache kuthibitika kuwa hawatokuwa na Neymar katika michezo yote miwili ya 16 bora ya klabu bingwa Ulaya dhidi ya Manchester United kwa majeruhi pia.
PSG sasa ina hatari ya kumkosa Edinson Cavani aliyeripotiwa kuumia jana katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Ufaransa.
Edinson Cavani katika mchezo huo dhidi ya Girondis Bordeaux wa Ligi Kuu ya nchini Ufaransa Ligue 1 aliumia dakika ya 46 na kushindwa kuendelea na mechi hiyo iliyomalizika kwa PSG kuondoka na ushindi wa 1-0 bao ambalo lilifungwa na Mruguayi huyo kwa mkwaju wa penati dakika ya 42.