Infantino kukalia kiti cha Urais bila kupingwa
Mtandao wa marca.com umeripoti kuwa Rais wa sasa wa shirikisho la mpira wa miguu ulimwenguni FIFA Gianni Infantino ataendelea kukalia kiti hicho cha Urais hadi mwaka 2023, hiyo ni baada ya Rais huyo kutopata wagombea wanaompinga katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania nafasi hiyo ya Urais wa FIFA.
Uchaguzi Mkuu wa shirikisho la mpira wa miguu duniani (FIFA ) umepangwa kufanyika June 5 2019 lakini hadi sasa hakuna mgombea yeyote aliyeripotiwa kujitokea kuchukua fomu na kumpinga Rais huyo katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka huu.
Sifa ya kugombea Urais wa FIFA ni lazima mgombea awe amehusika katika uongozi wa masuala ya soka katika kipindi cha miaka miwili ila pamoja na hayo uchaguzi ili ufanyike ni lazima mashirikisho wanachama matano yatoe wagombea kitu ambacho hakijatokea na kimya hicho kinaashiria kumuunga mkono Infantino.
Infantino ambaye amehudhuria mkutano wa UEFA Alhamisi hii amesema kuwa atagombea tena Urais wa FIFA katika uchaguzi mkuu wa June na tayari amepokea taarifa za kuungwa na mashirikisho ya soka 190 kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao ni wanachama wa FIFA japo UEFA bado hawajataja msimamo wao licha ya Afrika, Asia, Amerika ya Kati na Amerika Kusini wametaja.