Emiliano Sala apoteza maisha, polisi wathibitisha
Polisi wa Dorset leo wametoa taarifa za kusikitisha kwa familia ya mpira wa miguu kufuatia kutangaza kuwa mwili uliokuwa umekutwa kwenye mabaki ya ndege chini ya bahari ni mwili wa Emiliano Sala, taarifa hizo zimetolewa baada ya kufanyiwa uchunguzi katika maabara mchana wa Februari 7.
Emiliano Sala,28, aliyejiunga na Cardiff City ya nchini Wales siku mbili kabla ya kupotea na ndege akiwa na rubani wake David Ibbotson, alisajiliwa na Cardiff City kwa mkataba wa miaka mitatu kwa dau la pauni milioni 15 ila alipata matatizo baada ya kurudi kuwaaga wachezaji wenzake katika klabu yake ya Nantes FC ya Ufaransa.
Dunia ya soka sasa imepata msiba mzito wa nyota huyo raia wa Argentina ambaye alikuwa chaguo sahihi la kuziba pengo la safu ya ushambuliaji la timu ya Cardiff City ya nchini Wales ila inashiriki Ligi Kuu ya nchini England, Sala amezaliwa Cululu nchini Argentina 1990
Emiliano Sala ambaye amepoteza maisha kwa ajali ya ndege, hadi mauti yanamkuta alikuwa amewahi kuvichezea vilabu mbalimbali kama Orleans aliyoichezea michezo 37 kwa mkopo na kufunga magoli 19, Niort kwa mkopo akicheza michezo 40 na kufunga mabao 20, Bordeaux 12 na kufunga bao 1, Caen kwa mkopo na kufunga mabao 5 katika michezo 13 na Nantes FC aliyoichezea michezo 133 na kufunga mabao 48.