Zahera atupa lawama kwa waamuzi
Mwalimu wa Yanga SC mwenye uraia wa Congo na Ufaransa Mwinyi Zahera sasa ameanza kukutana na wakati mgumu katika Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2018/2019 baada ya kuanza kuona ugumu wa mechi za mikoani, Yanga jana walikuwa wamesafiri kwenda Tanga kucheza mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union.
Baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Coastal Union wakiwa wamepata sare ya kufungana goli 1-1, magoli yakifungwa na Haji Ugando kwa Coastal Union na Deus Kaseke kwa Yanga baada ya pasi nzuri ya usaidizi wa goli kutoka kwa Matheo Anthony, kocha wa Yanga Mwinyi Zahera ameendelea kulaumu kuwa mwamuzi wa mchezo ndio ameharibu mechi hiyo pasipokujua kuwa wenyewe wanatumia gharama kuendesha timu yao.
“Kesho tunasafiri kwenda Singida tutasafiri kwa saa nane na unatoka tena Singida unarudi hapa ukitumia tena saa nane unalipa hotel unakula, hiyo yote unatoa pesa halafu mtu huyu mmoja anaenda kuharibu mambo yote ni refa, TFF yenu hii na wale wa bodi ya Ligi vitu gani wanaitika vya hovyo hivi, wanatakiwa wajue timu haziwezi kuendelea hivi, hakuna cha uwanja mbaya uwanja ni wa timu zote mbili wachezaji wetu wanapaswa kuzoea uwanja, tulishinda mechi sita za ugenini mwanzoni na tulicheza viwanja vya hivi na tulishinda” alisema Mwinyi Zahera baada ya mchezo
Matokeo hayo sasa yanakua na presha kubwa kwa Yanga aliyekuwa awali anaongoza Ligi akiwa na alama ambazo hata kama mpinzani wake Simba akishinda michezo yake yote ya viporo bado angekuwa amemzidi alama tano ila baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union, Yanga sasa kama Simba atacheza na kushinda viporo vyake vyote atakuwa ana alama sawa na Yanga anayeendelea kuongoza Ligi kwa kuwa na alama 54 hadi sasa akifuatiwa na Azam FC wenye alama 47 na kiporo kimoja wakati Coastal Union wakiwa nafasi ya 8 kwa kuwa na alama 29 wakiizidi kwa tofauti ya magoli JKT Tanzania.