Wambura kumpeleka Karia Mahakamani
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania, Michael Wambura amesema atampeleka mahakamani Rais wa Shirikisho hilo Wallace Karia kwa kushindwa kuheshimu maamuzi yaliyotolewa na Mahakama kuu ya Tanzania.
Wambura amesema kuwa Rais Karia ndiye mtu aliyekiuka maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuu hivyo anamfikisha mahakamani kwa kosa hilo.
Ikumbukwe kuwa Machi 15,2018 kamati ya maadili ya TFF ilimfungia maisha Wambura kujihusisha na masuala ya soka
kutokana na kutuhumiwa kwa makosa matatu ambapo moja ni kupokea pesa za TFF isivyo halali, kugushi nyaraka na kosa la tatu kushusha hadi ya shirikisho hilo.
Disemba 4 Wambura aliambatana na mwanasheria wake Emmanuel Muga aliwasilisha hati ya Mahakama Kuu ya Kupinga kufungiwa kwake maisha kwa kutokujihusisha na masuala ya soka na kudai kamati ya maadili ya TFF ilikiuka baadhi ya kanuni wakati wa kumfungia kwake hivyo, Mahakama ilitengua maamuzi ya kamati ya maadili ya kumfungia Kiongozi huyo.
Januari 23 mwaka huu TFF kupitia kamati yake ya nidhamu ilitangaza tena kumfungia maisha Wambura kujihusisha na masuala ya soka baada ya FIFA kupitia kamati yake ya nidhamu chini ya mwenyekiti wake Anin Yeboah wa Ghana kukazia hukumu ya kamati ya rufani ya maadili ya TFF iliyotolewa April 6,2018.