Sala ataka kumstaafisha kocha Cardiff
Jiji la Cardiff hadi sasa limetawaliwa na huzuni na simanzi kuhusiana na tukio la kupotea kwa ndege ndogo binafsi iliyokuwa imembeba mchezaji mpya wa Cardiff City Emiliano Sala akiwa na rubani wake David Ibbotson ambaye alikuwa akisafiri nae kutokea Nantes Ufaransa kurejea Cardiff.
Baadhi ya watu wamekata tamaa kuhusiana na kupotea kwao huko kufuatia watu wa uokoaji awali kutangaza kuwa hakuna matumaini ya watu hao kupatikana wakiwa hai, hiyo ilikuwa siku moja kabla ya Polisi na kikosi kazi cha uokoaji kutangaza kuwa wamesitisha zoezi hilo baada ya kuitafuta ndege hiyo ardhini na nchi kavu kwa saa 80 bila mafanikio.
Wakati zikitangazwa taarifa za kuanza upya kwa zoezi binafsi la utafutaji wa ndege hiyo kufuatia kupatikana michango ya zaidi ya euro 300000 zilizochangwa na watu zaidi ya 4000, kocha mkuu wa Cardiff City Neil Warnock ametangaza jambo la kushangaza kidogo kufuatia tukio la kupotea kwa mchezaji wake Emiliano Sala.
Neil Warnock mwenye umri wa miaka 70 ambaye amedumu katika kazi ya ukocha kwa takribani miaka 40 amesema anafikiria kustaafu kazi ya ukocha kutokana na tukio hilo lililotokea, Neil Warnock anasema amekuwa na wiki ngumu sana katika maisha yake ya ukocha toka. .
“Nimekuwa katika kazi ya uongozi wa soka kwa miaka 40 sasa, ninafikiri hiki ndio kipindi change kigumu kuwahi kupitia katika kazi hii, nikimuangalia Romina (Dada wa Sala) na familia yao najua wapo katika wakati mgumu, ninawafikiria watoto wangu ningefanyaje sasa kama ingenitokea mimi vile vile, kuhusu kustaafu kwa hili nilifikiria karibia saa 24 kwa siku wiki iliyopita hata hapa nilipo hilo nalifikiria” alisema kocha Neil Warnock