KIPIGO CHA KOREA KUSINI ASIA CUP KIMEPELEKA FARAJA TOTTENHAM
Baada ya kuwa na mfululizo wa majeruhi katika kikosi cha Tottenham Hotspurs chini ya kocha wao Pochetinho leo wamezipokea taarifa njema ambazo zitaleta ahueni katika kikosi hicho cha Spurs, jana zimeripotiwa taarifa za mchezaji wao raia wa Korea Kusini Son Heung-min yuko mbioni kurudi.
Son Heung-min alikuwa nje ya kikosi cha Tottenham kufuatia kuwa na majukumu ya kuitumikia timu yake ya taifa ya Korea Kusini katika michuano ya Asian Cup iliyomalizika kwa Korea Kusini kutolewa na Qatar katika hatua ya robo fainali kwa kufungwa bao 1-0 licha ya awali kupewa na nafasi kutwaa taji hilo.
Pamoja na kuwa Korea Kusini waliutawala mchezo zaidi ya Qatar lakini walijikuta wakikata tiketi rasmi ya kuyaaga mashindani hayo dakika ya 78 kufuatia mchezaji wa Qatar Abdulaziz Hatem kufunga goli la ushindi lililoipa tiketi Korea na kuipeleka Qatar kucheza hatua ya nusu fainali.
Kurejea kwa Son Heung-min kutaleta faraja na matumaini ya kufanya vizuri kwa Tottenham katika michuano mbalimbali licha ya kuwa wameshatolewa katika michuano ya Carabao Cup, hivyo atapunguza machungu kwa kocha wao ambaye anapata tabu kukosekana kwa wachezaji wake muhimu kama Dele Alli, Harry Kane na Victor Wanyama kuwa majeruhi.