Lineker achukizwa na Monaco
Uongozi wa timu ya AS Monaco ya nchini Ufaransa umeamua kumsimamisha kazi kwa muda usiojulikana kocha mkuu wa timu hiyo mfaransa Thierry Henry, uongozi ulitangaza taarifa hizo baada ya mfululizo wa matokeo mabovu ya timu hiyo ambayo ipo nafasi ya pili kutoka mwisho.
Baada ya Henry kusimamishwa uongozi unasubiri kukaa na kujadili hatma ya kocha huyo aliyedumu na timu hiyo kwa miezi mitatu na kuiongoza katika michezo 20, wakishinda 4, sare mitano na wamepoteza mara 11, hivyo timu ipo katika sehemu za hatari kushuka daraja na kwenda Ligue 2.
Kutokana na kitendo cha kocha kusimamishwa sio cha kawaida na wengi wamezoea kuona kocha akikosea anafukuzwa kazi au uongozi usiporidhishwa na utendaji wake anafukuzwa kazi, mchambuzi wa masuala ya soka Gary Lineker amelikosoa jambo hilo na kuliita ni udhalilishaji kwa mkongwe huyo wa soka.
.
“Ona Thierry Henry amesimamishwa kufanya majukumu yake ya kufundisha AS Monaco kuna minong’ono kuwa klabu inajidili namna ya kufanya na Henry, hiyo inaonekana kama unamdhalilisha na kumkosea heshima legend kama yeye kumfanyia hivyo, kama unataka kumfukuza kazi mfukuze kazi tu” aliandika Lineker katika ukurasa wake wa twitter saa kadhaa baada ya taarifa hizo kutoka.