Ismaily yatolewa Klabu Bingwa na CAF
Timu ya Ismaily ya nchini Misri ambayo hivi karibuni ilifanikiwa kumsajili mchezaji wa kitanzania Yahaya Zayd katika timu yao kwa ajili ya kuongeza nguvu katika mashindano mbalimbali zimetoka taarifa mbaya kutoka CAF Kuhusu timu hiyo.
Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) limefikia maamuzi ya kuitoa Ismaily katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyooneshwa na mashabiki wao wakati wa mchezo wa klabu Bingwa Afrika Januari 18 nyumbani dhidi ya timu ya Club Africain ya Tunisia.
CAF wametangaza kuiadhibu timu hiyo kwa kuitoa katika mashindano hayo baada ya kamishna wa mchezo huo kuandika katika ripoti yake kuwa mashabiki wa timu ya Ismaily walikuwa wakirusha mawe kwa wachezaji wa timu pinzani na kwa mwamuzi msaidizi wa mchezo, ndipo dakika ya 86 mchezo ukavunjika na waamuzi wakatolewa uwanjani wakisindikizwa na watu wa usalama.
Wakati mchezo unavunjika Club Africain walikuwa wanaongoza kwa goli 2-1.
Kundi C sasa linabaki na timu za CS Costantine, Club Africain na TP Mazembe.