Baraza achukua hatamu Sofapaka
Mwenyekiti wa klabu ya Sofapaka Elly Kalekwa amedhibitisha kuteuliwa kwa John Baraza kama kocha mkuu baada ya kuondoka kwa Melis Medo.
Medo alifutwa kazi na Sofapaka hivi majuzi na Baraza ambaye alikuwa kocha msaidizi amerejea kileleni kwa mara ya tatu.
Mwaka wa 2016 alichukua hata baada ya kufurushwa kwa David Ouma na mwaka wa 2018 aliichukua nafasi yake Sam Ssimbwa aliyejiuzulu.
Kulingana na Kalekwa, Baraza ambaye alikuwa nahodha na mshambulizi wa Sofapaka hapo awali amepewa majukumu ya kuiongoza timu hiyo kwa kandarasi ya kudumu.
“Baraza anatosha kuiongoza timu hii. Mkikumbuka vyema ni yeye aliyetusaidia tusishushwe daraja mwaka wa 2016. Tutamtafutia kocha msaidizi na Nina imani kuwa ataiongoza timu hii vyema,” alisema Kalekwa.
Sofapaka ilicheza sare ya sufuri kwa sufuri siku ya Jumamosi ugani Kenyatta, Machakos.