AZAM FC WALIA MECHI YAO NA YANGA KUPIGWA DANADANA
Klabu ya Azam FC yenye maskani yake Mbande Chamazi Dar es Salaam, kupitia kwa afisa habari wake Jafari Iddi wameelezea masikitiko yao juu ya uamuzi wa bodi ya Ligi kuahirisha mchezo wao dhidi ya Yanga kwa sababu ambazo wanaamini hazina mashiko.
Azam FC wameanza mechi za mzunguuko wa pili wakiwa tayari wana viporo vya michezo ya mzunguuko wa kwanza dhidi ya Simba na Yanga ila kuwa na kiporo dhidi ya Simba hawana neno kwa kuwa sababu zao zinaeleweka wana michezo ya kimataita ila kwa upande wa Yanga ndio hawaelewi kutokana na Yanga alitolewa Mapinduzi Cup mapema hivyo hawaoni sababu za mchezo huo kupigwa danadana.
“Cha-kushangaza sisi tunakwenda round ya pili wakati tuna mechi za round ya kwanza na Yanga wako hapa, Yanga tulikuwa nao Zanzibar kwenye mashindano wametolewa mapema na wamerudi hapa muda mrefu kwa nini tusimalize mechi yetu na Yanga kwanza halafu ikabakia mechi yetu na Simba ndio twende round ya pili halafu baadae wangetupangia hiyo round ya pili baada ya Simba kurudi tungemaliza” alisema Jafari Iddi
“Kusema kweli imetusikitisha na haipendezi unaendaje katika hatua nyingine wakati bado tuna mechi nyingine hapa na klabu ambazo tungecheza nazo moja ipo hapa kiukweli hayo ni masikitiko yetu katika ratiba ya Ligi Kuu Tanzania bara” alisema Jafari Iddi
Azam FC ambao ndio Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa mara ya tatuu mfululizo, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2018/2019 wapo nafasi ya pili wakiwa na alama 41 na kacheza michezo 18, Yanga akiongoza kwa kuwa na alama 53 akiwa kacheza michezo 19, wakati Simba ikiwa nafasi ya nne kwa kuwa na alama 33 ila ila imecheza michezo 14 pekee.