MWANDISHI ALIYEGUNDUA RUSHWA KATIKA SOKA LA GHANA KAUWAWA
Kutoka nchini Ghana leo zimeripotiwa taarifa za kuuwawa kwa risasi kwa mwandishi wa habari za kiuchunguzi Ahmed Hussein Suale kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, tayari polisi nchini Ghana wameripoti kuwa uchunguzi wa mauaji ya mwandishi huyo umeanza mara moja.
Ahmed Hussein ambaye mwaka jana aliteka vichwa vya habari katika soka la Afrika baada ya kuchunguza madudu na ufisadi uliyokuwa unafanyika katika soka la Ghana kiasi cha kupelekea kujiuzulu na kufungiwa maisha kujihusisha na soka kwa Rais wa chama cha soka nchini Ghana, ameadaiwa kuuwawa na watu waliyokuwa kwenye boda boda.
Hata hivyo Ahmed Hussein Suale kazi yake ilipata umaarufu mkubwa Afrika Mashariki baada ya kufanikiwa kufanya habari ya kichunguzi na kumnasa muamuzi msaidizi wa Kenya Aden Range Marwa akipokea rushwa ya dola 600, kitu ambacho kilipelekea muamuzi huyo kufungiwa maisha kujihusisha na soka na kuondolewa katika orodha ya waamuzi wasaidizi waliyokuwa wamechaguliwa kusimamia Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.