Foster amkubali de Gea
Mlinda mlango wa timu ya Watford ya nchini England Ben Foster ameeleza mtazamo wake kuhusiana na mawazo ya watu mbalimbali waliokuwa wanajadili kuhusiana na uwezo aliouonesha mlinda mlango wa Manchester United David De Gea katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tottenham Hotspurs.
Pamoja na kuwa mchezo huo ulimalizika kwa Manchester United kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini lililofungwa na Marcus Rashford dakika ya 44, lakini Manchester United ilizidiwa mchezo na hali ya kumiliki mpira kitu ambacho kiliifanya Tottenham kuwa na nguvu ya kuishambulia Manchester United zaidi.
Jitihada za David De Gea ndio ziliiokoa Manchester United kutokana na umahiri wake akiwa langoni la sivyo wangeweza kuruhusu magoli zaidi ya moja, kwenye mchezo huo pekee David De Gea aliiokoa mipira ya hatari 11 ambayo bila umakini wake ingeweza kutinga nyavuni, hivyo Ben Foster kaamua kueleza kitu ambacho inawezekana watu hawafahamu kuhusiana na uwezo wa David De Gea.
.
“Nimeona watu wengi wakijadili kuhusiana na mipira aliyoiokoa David De Gea kuwa ilikuwa inamlenga moja kwa moja ndio maana akawa anaiokoa, ukweli ni kwamba jamaa (De Gea) ana uwezo wa kujua awe sehemu gani golini na kwa wakati muafaka, hiyo huwezi kuifundisha ni ipo tu kwa mchezaji mwenyewe” alisema Ben Foster kwa wale wanaokosoa kuwa De Gea ameweza kucheza mipira hiyo kwa sababu ilimfuata.