Genk wakataa kumuuza Samatta
Nyota wa kitanzania anayecheza soka katika timu ya KRC Genk ya nchini Ubelgiji Mbwana Samatta, anaendelea kuwindwa na timu mbalimbali barani Ulaya kwa ajili ya uhamisho wa dirisha dogo la usajili la mwezi Januari, Samatta kwa sasa anahitajika na klabu ya Cardiff City inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini England.
Klabu ya Cardiff City imeripotiwa na mtandao wa hitc.com kutoa ofa ya dau la pauni milioni 11.6 ( Tsha Bilioni 34) kwenda KRC Genk ili kuishawishi timu hiyo iwauzie Mbwana Samatta ambaye wanaamini atakuwa mkombozi katika kikosi chao ambacho kipo katika nafasi za hatari za kushuka daraja kama kikiendelea kusuasua.
Genk wameripotiwa kulikataa dau hilo la Cardiff.
Samatta anatajwa kuwa msaada sahihi kwa Cardiff kutokana na mchezaji huyo kuendelea kuonesha kiwango cha juu akiichezea Genk michezo 31 ya mashindano yote msimu huu na kupasia nyavu mara 24 katika michezo hiyo.
Cardiff kwa sasa ipo nafasi ya 17 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 19 tofauti ya alama moja na Newcastle ilipo nafasi ya 18 ya kushuka daraja.