LOUIS VAN GAAL KAIPA LIVERPOOL UBINGWA WA UINGEREZA
Pamoja na kuwa timu ya Liverpool hivi karibuni ilipoteza katika mchezo wake wa Ligi Kuu ya nchini Uingereza dhidi ya Manchester City katika uwanja wa Etihad kwa mabao 2-1, kocha wa zamani wa Manchester United Louis van Gaaal ametabiri kuwa timu hiyo ndio bora na itatwaa Ubingwa wa Uingereza dhidi ya Manchester City msimu huu.
Louis van Gaal amefika mbali na kueleza kuwa kocha wa Manchester City Pep Guardiola anafundisha kushambulia ila anaamini Liverpool mpaka kufikia mwezi Mei itakuwa Bingwa wa Uingereza ila kwa upande wa Manchester City anabaki na kuendelea kuamini tu timu hiyo ina wachezaji wazuri.
“Kama nataka kuweka hela na kubashiri nani atakuwa Bingwa wa Ligi Kuu Uingereza basi ningeweka kwa Liverpool, timu ya Liverpool ipo kwenye viwango vya juu ila linapokuja suala la mchezaji mmoja mmoja basi Manchester City wana wachezaji wenye viwango sana, kwa upande wa udhaifu wa Guardiola katika kikosi chake ni kwamba anakifundisha kushambulia zaidi” alisema Louis van Gaal
Manchester City hadi sasa ndio timu pekee Uingereza iliyofunga magoli mengi msimu huu, ikipasia nyavu mara 56 wakati wapinzani wao katika mbio za Ubingwa wa Ligi Kuu Liverpool wakifunga mara 49, hadi sasa timu hizo katika Ligi Kuu Uingereza zimetofautiana alama 4 Liverpool akiwa kileleni kwa alama 54 na Manchester City akifuatia kwa kuwa na alama 50, tukukumbushe tu Louis van Gaal alikuwa kocha wa Manchester United kwa miaka miwili (2014-2016) na kufutwa kazi mwaka 2016 na mikoba kupewa Mourinho. Aliyedumu nae kwa miaka miwili tu (2016-2018)