DIEGO MARADONA AUNGANA NA KALIDOU KOULIBALY
Jina la Diego Maradona ni miongoni mwa majina makubwa katika soka na kiuhalisia ni kwamba ukizungumzia magwiji wa soka duniani huwezi kuacha kumtaji Diego Maradona wa Argentina na gwiji mwenzake wa Brazil Pele, ukubwa wa majina yao umetokana na mambo makubwa waliyokuwa wanayafanya uwanjani enzi hizo.
Hivi karibuni katika mchezo wa Inter Milan dhidi ya Napoli uliyochezwa katika uwanja wa Sansiro na kumalizika kwa Inter Milan kupata ushindi wa bao 1-0, zilisikika kelele za mashabiki wa Inter Milan wakimtolea maneno ya kibaguzi mlinzi wa kati wa kimataifa wa Senegal anayeichezea Napoli ya nchini Italia Kalidou Koulibaly.
Kalidou Koulibaly katika mchezo huo ambao kocha wake Ancelotti aliomba uahirishwe kutokana na kupigiwa kelele za nyani, nyota kadhaa wa soka walionekana kuguswa na kuamua kutumia kurasa zao za twitter kupinga ubaguzi wa rangi aliyofanyiwa Kalidou Koulibaly.
Maradona ameamua kuonesha masikitiko yake kuhusiana na kitendo alichofanyiwa Koulibaly na kuamua kushika jezi ya mchezaji huyo na kusema kuwa hata yeye aliwahi kukumbana na hali kama ya Koulibaly alipokuwa mchezaji, hivyo aliamua kuwasilisha hisia zake kwa kupiga picha akiwa kashika jezi ya Koulibaly na kuishea katika ukurasa wake wa instagra, tukukumbushe tu Maradona pia amewahi kucheza Napoli kwa miaka 7 kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1991 na kuamua kwenda kujiunga na Sevilla alikodumu kwa miaka miwili.