AZAM FC WAMETANGAZA KWENDA MOROGORO KULINDA REKODI YAO
Klabu ya Azam FC imesafiri kuelekea Manungu Turiani kucheza mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania bara dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi tarehe 29, Disemba 2018 wakiwa wanaenda kutetea rekodi yao imara ya kutopoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu Msimu huu.
Azam FC kupitia msemaji wao Jaffari Iddi Maganga amethibitisha timu hiyo kusafiri kuelekea mjini Morogoro na kuthibtisha kuwa wanaenda kulinda rekodi yake ya kutopoteza mchezo wowote wa Ligi Kuu wakiwa hawana majeruhi.

Hata hivyo Azam FC pia imethibitisha kuwa mchezaji wao mahiri Frank Raymond Domayo aliyekuwa anasumbuliwa na mejeraha kwa muda mrefu amerejea uwanja na sasa ameanza mazoezi mepesi mepesi chini ya uangalizi wa makocha na madaktari wa timu hiyo

“Sisi kama Azam FC tumejiadndaa vizuri kuhakikisha tunaenda kupambana na Mtibwa Sugar ni mchezo mgumu bila shaka lakini mwalimu Hans na Mwambusi wameiandaa timu vya kutosha kuweza kupamba na Mtibwa lakini kumbuka tu Azam hadi sasa ni timu ambayo haijapoteza mchezo, mchezaji nguli ambaye alikuwa majeruhi Frank Domayo tayari ameanza mazoezi mepesi kujiandaa dhidi ya michezo mbalimbali ya Ligi Kuu kikosi kinaondoka bila kuwa na majeruhi”alisema Jaffar
Kwa sasa Azam FC katika msimamo wa Ligi Kuu nchini inashika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga wanaoongoza Ligi, Yanga wapo nafasi ya kwanza wakicheza michezo 17 na kuwa na alama 47 wakati Azam FC wapo nafasi ya pili kwa kuwa na alama 40 ila wamezidiwa mchezo mmoja na Yanga wao Azam FC wakicheza michezo 16.