KAULI YA SAMATTA KATIKA USHINDI WA 2-0 DHIDI YA KAS EUPEN YEYE AKISHINDA MAWILI
Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars na kinara wa mabao wa Ligi Kuu ya nchini Ubelgiji Mbwana Samatta baada ya kuwa sehemu ya kikosi cha timuya KRC Genk kilichopata ushindi wa 2-0 katika uwanja wa ugenini dhidi ya KAS Eupen, Samatta kafunguka
Samatta ambaye ana siku ya nne le toka asaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea na KRC Genk, ndio alifunga mabao yote mawili katika ushindi dhidi ya KAS Eupen, mabao hayo akiyafunga dakika ya 13 na 20 na kuendelea kuwa kinara wa ufungaji wa Ligi kwa kufikisha mabao 14 tofauti ya mabao matatu na wanaomfuatia.
“Najisikia vizuri kwa sababu yalikuwa ni mabao mazuri kwa ajili ya kusaidia timu yangu kupata ushindi leo, alama tatu ni muhimu tena pale unaposhinda katika mchezo wa ugenini inakupa nguvu ya ziada, imekuwa ni kawaida kuangali michezo iliyopita kama tumepoteza tunaangalia tumekosea wapi” alisema Samatta alipohojiwa na Genk TV
Ushindi huo umeiweka KRC Genk kwenye ramani nzuri ya kuendelea kuwania Kombe la Ligi Kuu nchini Ubelgiji, wakiongoza kwa alama 45 kwa 38 dhidi ya Club Brugge wanaofuatia Genk wakiwa wamecheza michezo 20, wameshinda 13, sare michezo 6 na wamefungwa mchezo mmoja tu.